Vyama Uturuki vyalalamikia ajali mgodini

Haki miliki ya picha bbc
Image caption Kilio cha jamaa na familia za waathiriwa

Polisi nchini Uturuki wametumia gesi ya kutoa machozi na magari ya maji kuwatawanya maelfu ya waandamanaji katika mji wa magharibi wa Izmir.

Waandamanaji wanafanya mgomo wa siku moja ulioitishwa na viongozi wa vyama vya kutetea wafanyikazi kulalamikia mkasa mbaya zaidi wa mlipuko katika mgodi wa mawe uliotokea nchini humo.

Waandamanaji walikusanyika katika barabara moja na kuwazomea maafisa wa polisi wakati walipokuwa wakitumia magari ya kuwamwagia maji kujaribu kuwatawanya.

Kuna ripoti za kutokea maandamano zaidi katika miji ya Istanbul, Diyarbakir na miji mingine.

Rais wa Uturuki, Abdullah Gul, anazuru eneo la mkasa huo ambako waokoaji bado wanaendelea kuwafikia zaidi ya wachimba migodi miamoja ambao bado wamekwama.

'Malalamiko kuhusu migodi'

Viongozi wa vyama vya wafanyakazi wanalalamika kuwa kuuzwa kwa migodi ya umma kwa watu binafsi kumechangia pakubwa katika kudorora kwa hali ya usalama katika viwanda.

Haki miliki ya picha
Image caption Wafanyakazi katika mgodi wakimsindikiza mmoja wao kutoka eneo la ajali hiyo ya Mgodi Soma.

Hadi kufikia sasa miili ya wafanyakazi 278 wa migodi imetolewa kwenye mgodi huo ulioko Soma.

Makundi ya waokozi yangali yanajaribu kuwafikia zaidi ya wafanyakazi wengine 100 ingawa juhudi zao zingali zinavurugwa na mioto inayowaka kwenye maeneo ya mgodi huo.

Waokoaji wenyewe imelazimu watibiwe kwa uchovu na kupumua moshi.

Mwandishi wa BBC katika Soma anasema kuwa baadhi familia za waliofariki wamekasirishwa na hatua ambazo zimechukuliwa na Serikali kufikia sasa.

Jumanne polisi walipambana na waandamanaji katika miji ya Ankara na Istanbul na Waziri Mkuu Recep Tayyip Erdogan alizomwa alipotembelea eneo la ajali hiyo ya mgodi.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii