Kuinyooshea mkono Sudan Kusini.

Haki miliki ya picha
Image caption Mamilioni Sudan kusini wanakabiliwa na njaa

Wajumbe wa kimataifa wanakutana katika kongamano mjini Oslo Norway, kuchanga fedha za kuisaidia Sudan Kusini inayokumbwa na mapigano kwa takriban miezi minne sasa.

Umoja wa mataifa unasema dola bilioni 1.26, zinahitajika kuwasaidia mamilioni ya watu katika taifa hilo changa Afrika, wanaokabiliwa na njaa.

Kwa mujibu wa Umoja huo, takriban raia milioni saba wa nchi hiyo huenda wakahitaji usaidizi wa kibinadamu.

Hali imezidi kuwa nzito kutokana na uwezekano wa kuwadia kwa msimu wa mvua utakaosababisha kutoweza kutumika kwa barabara chache zilizopo, na maeneo ya kutuwa ndege.

Hilo litatatiza usafirishaji wa misaada katika maeneo mengi nchini humo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mapigano yamewaacha wengi bila makaazi

Msaada uliotolewa

Hapo jana Norway, Denmark, na Marekani zilitangaza kujitolewa kifedha, kusaidia kuepusha janga hilo.

Rais Barack Obama ametangaza kwamba Marekani itaongeza dola milioni 50 kusaidia kutatua tatizo linaloongezeka la ukimbizi Sudan kusini.

Norway imetangaza msaada wa dola milioni 63 na awali Denmark iliahidi dola milioni10.

Haki miliki ya picha
Image caption Rais Kiir na Riek Machar wakikubaliana kusitisha mapigano

Bado mataifa kadhaa yanatarajiwa kuitikio ombi hilo la Umoja wa mataifa.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini ameonya kuwa taifa lake linakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kufuatia vita vikali vinavyoendelea.

Amemshutumu Riek Machar, kwa kuchochea mvutano wa kikabila baina ya makabila ya Nuer na Dinka, na kwenda kinyume na makubaliano ya kusitisha mapigano, yalioidhinishwa Addis Ababa mapema mwezi huu.

Sudan kusini ilikuwa taifa huru mnamo mwaka 2011 baada ya vita vilivyosababisha umwagikaji damu kati ya Sudan na kundi la waasi la Sudan People's Liberation Movement (SPLM), ambalo kwa sasa ndio lililomo serikalini.