Wanafunzi kambini Syria kufanya mitihani

Haki miliki ya picha
Image caption Mashambulizi mjini Yarmouk, Syria

Makubaliano yamefikiwa nchini Syria ili kuwarusu wanafunzi wanaoishi katika kambi ya wakimbizi inayoshuhudia mapigano makali ya Yarmouk viungani mwa mji wa Damascus kufanya mitihani yao ya kitaifa.

Baada ya majadiliano kati ya makundi hasimu vijana 120 waliweza kuruhusiwa kuondoka katika kambi hiyo kwa mda wa wiki mbili ili kufanya mitihani yao.

Mwandishi wa BBC amesema kuwa baada ya vijana hao kutoka nje ya kambi hiyo ya Yarmouk kulikuwa na hisia miongoni mwa jamaa na familia baadhi wakitokwa na machozi kwa kuwaona wanao.

Walizungumza kuhusu mazingira mabaya waliokuwa wakiishi na kula hata nyasi huku wakiishi na hofu ya kuzuka kwa ghasia.

Baada ya mtihani huo watalazimika kurudi katika kambi hiyo.

Kambi hiyo inayodhibitiwa na waasi ilizungukwa na jeshi tangu msimu wa joto na hivyobasi kusababisha ukosefu wa chakula.

Umoja wa mataifa unasema kwamba zaidi ya watu 100 wamefariki kutokana na magonjwa yanayosababishwa na njaa.