26 wauawa katika shambulizi Borno,Nigeria

Haki miliki ya picha BBC World Service

Kundi la wapiganaji wa kiisilamu la Boko Haram wametuhumiwa kwa kuwaua watu 26 katika mashambulizi dhidi ya kijiji kimoja Kaskazini Mashariki mwa Nigeria , karibu na eneo ambalo wasichana zaidi ya miambili walitekwa nyara.

Watu waliokuwa wamejihami waliwaua watu tisa katika kijiji cha Shawa na wengine kumi na saba katika kijiji cha Alagarno.

Eneo hilo liko karibu na mji wa Chibok ambako wasichana zaidi ya miambili walitekwa nyara mwezi jana na kundi la Boko Haram.

Hili ni shambulizi la hivi karibuni kufanywa nchini Nigeria wakati nchi hiyo ikikumbwa na kitendawili cha kuwatafuta zaidi ya wasichana miambili waliotekwa nyara na Boko Haram.

'Wataalamu wa kimataifa'

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mashambulizi yaliyofanywa awali na Boko Haram katika mji wa Jos

Juhudi hizo zinawashikirisha wataalamu wa ujasusi wa kimataifa kutoka Israel, Marekani na Uingereza.

Pia limetokea siku moja tu baada ya milipuko miwili kutokea mjini Jos katika jimbo la Plateau ambapo takriban watu 118 waliuawa Jumanne usiku.

Juhudi za kuwatafuta maiti bado zinaendelea.

Mwandishi wa BBC nchini Nigeria anasema kuwa shambulizi lililofanyika mjini Jos, lilisababishwa na Boko Haram na kwamba huenda ni ujumbe kwa serikali kuwa wapiganaji hao wanaweza kushambulia wakati wowote wanapotaka.

Wanakijiji wanasema kuwa wapiganaji hao walisawili katika kijiji hicho usiku wa manane na kuwalazimisha watu kutoroka na kujificha vichakani.

Inaarifiwa waliondoka baada ya saa nne za usiku wakiwa wamebeba chakula walichoiba pamoja na magari.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii