Marekani yatuma wanajeshi wake Chad

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Boko Haram liliwateka wasichana takriban 200 wa shule mwezi uliopita

Marekani inatuma wanajeshi wake nchini Chad ili kusaidia kuwatafuta na kuwaokoa takriban wasichana 200 waliotekwa nyara nchini Nigeria.

Watoto hao wa shule, walichukuliwa na kundi la Boko Haram, ambalo ni kundi la wanamgambo wenye msimamo mkali wa Kiislamu wanaopinga masomo ya nchi za magharibi.

Kwa kutumia nguvu zake za kivita, Rais Barack Obama aliamuru kutumwa kwa wanajeshi, kama sehemu ya jitihada za Marekani, kuwatafuta na kuwarejesha wasichana hao kwa familia zao.

Katika barua kwa bunge, ikulu ya White House ilisema kwamba wanajeshi hao 80, watasaidia katika upelelezi, ukaguzi na katika operesheni za ndege angani, kaskazini mwa Nigeria na maeneo yanayolizunguka eneo hilo.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Wanajeshi wataisaidia katika kuwatafuta na kuwaokoa wasichana hao

Wanajeshi hao watakua na makao yao Chad na watasalia huko hadi pale ambapo hawatahitajika tena.

Chad inapakana na Nigeria, sehemu ambayo wasichana hao 276 walitekwa na Boko Haram, mwezi uliopita.

Katika kanda moja ya video, kundi hilo linatishia kuwauza wasichana hao katika utumwa, iwapo serikali ya Nigeria haitawaachilia huru wanamgambo waliopo gerezani.

Nchi nyingi zimeahidi kuisaidia Nigeria baada ya Rais Goodluck Jonathan kushutumiwa kwa ulegevu katika kukabiliana na utekaji nyara huo.