Jeshi Thailand lamuhifadhi Bi Shinawatra

Bi Yingluck Shinawatra Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waziri mkuu wa Thailand aliyepinduliwa Bi Yingluck Shinawatra

Kiongozi wa Thailand aliyeng'olewa madarakani Yingluck Shinawatra ameonekana katika kituo cha jeshi mjini Bangkok, siku moja baada ya jeshi kunyakua mamlaka kwa njia ya mapinduzi.

Bi Yingluck ni mmoja kati ya wanasiasa 100 walioitwa na jeshi .

Jesi limewawekea vikwazo vya kwenda nje ya nchi wanasiasa 155 mashuhuri bila ruhusa.

Aidha hapo jana (Alhamis) jeshi lilitangaza kuahirisha katiba, kuzuia mikusanyiko na kuwatia nguvuni wanasiasa , likisema hali ya utulivu inahitajika baada ya kipindi cha mwezi mmoja cha ghasia.

Leo inaelekea kuwa Bi Yingluck ameondoka kwenye kituo cha jeshi alikoitwa na kupelekwa kwenye kituo kingine cha kijeshi, mwandishi wa BBC Jonah Fisher amearifu kutoka Bangkok.

Kwa mujibu wa mwandishi wetu, haijabainika wazi ikiwa bado amewekwa lumande au la , anasema ripota wetu .

Viongozi wa chama chake cha Pheu Thai na kile cha upinzani cha Democrats kwa pamoja waliachiliwa huru kutoka mahabusu ya kijeshi usiku wa kuamkia leo

Hata hivyo , kiongozi wa waandamanaji wanaaminiwa kuwa bado wako mahabusu na baadhi ya wabunge wa serikali wamekwenda mafichoni.