Watoto waasiliwa na wapenzi wa jinsia moja

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Mahakama kuu mjini London

Wazazi wenye uraia wa Slovakia walioshindwa kuwalea watoto wao wawili wameshindwa kuwazuia wapenzi wawili wa jinsia moja mjini Kent Uingereza kuwaasili watoto hao.

Wazazi hao wanaoishi nchini Uingereza na ambao ni waumini wa kanisa katoliki, walipinga kitendo hicho cha kuasiliwa kwa watoto wao wakisema kuwa watakuwa mbali na familia pamoja na jamii yao

Waliwasilisha malalamiko yao katika mahakama kuu wakituhumu maafisa wa baraza la jiji kwa kuwapeleka mbali watoto wao na kutaka kuwageuza watoto kuwa waingireza na kuishi maisha ambayo hawajazoea.

Hata hivyo ushahidi uliokuwa umetolewa dhidi ya wazazi hao ulionyesha kwamba walikuwa wameshindwa kuwalea watoto wao

Katika kile ambacho jaji alitaja kuwa kisa cha kuhuzunisha, watoto hao wavulana mmoja akiwa na umri wa miaka minne na mwingine miwili, walikabidhiwa wapenzi hao wa jinsia moja kutoka Uingereza baada ya maafisa kusema kuwa wazazi wao wanawapuuza watoto wao.

Hata hivyo jaji alifikia uamuzi wake baada ya kusema kuwa wazazi hao hawakuwa tayari kukubali kukosolewa na kwamba hawakua tayari kubadili mienendo yao na kuwa wazazi wazuri kwa watoto wao.

Mahakama iliarifiwa kuwa watoto hao hawakuwa wakienda shule , waliachwa peke yao mara kwa mara na baba yao pia alikiri kuwachapa na wakati mwingine mwenyewe kuwa mchafu sana.

Jaji alisema watoto hao wanapaswa kuasiliwa kwa mustakabali wao mwema.

Lakini wazazi walipinga mahakama kuruhusu watoto hao kuasiliwa na wapenzi wa jinsia moja

Walisisitiza kuwa swala la mapenzi ya jinsia moja halitambuliwi na kanisa katoliki na limekewema sana na mapadri wa Slovakia.

Pia walisema kuwa kuruhusu wapenzi wa jinsia moja kuwaasili watoto wao, kutawaathiri baaaye maishani.