Wahariri watakiwa kufika mbele ya jeshi

Haki miliki ya picha AP
Image caption Maafisa wakuu wa jeshi nchini Thailand wakizungumza na vyombo vya habari

Serikali ya jeshi nchini Thailand imewataka wahariri wanane wa magazeti nchini humo kufika mbele yake baadaye hii leo.

Mwandishi wa BBC mjini Bangkok amesema kuwa mkutano huo unatarajiwa kuwa majadiliano ya upande mmoja kuhusu walivyoripoti habari za mapinduzi ya wiki iliopita.

Serikali ya jeshi pia imewaonya raia wake kutoshiriki katika maandamano dhidi ya mapinduzi hayo.

Msemaji wa jeshi mjini Bangkok amesema kuwa sera za kidemokrasi haziwezi kutekelezwa wakati kama huu.

Msemaji huyo pia alitetea kukamatwa kwa wanasiasa na wanaharakati akisema wanazuiliwa ili kujenga ufahamu wa mzozo huo.

Siku ya jumamosi watawala hao walivunja bunge la sineti ambalo lina uwezo wa kukabiliana na serikali hiyo ya jeshi.