Raia washiriki katika uchaguzi Ukraine

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mwanajeshi wa Ukraine

Raia wa Ukraine wanashiriki katika uchaguzi wa urais nchini humo uliotajwa kuwa muhimu katika historia ya taifa hilo.

Hatahivyo haijulikani iwapo uchaguzi huo utafanyika katika maeneo mengine ya Ukraine ambapo wanamgambo wanaounga mkono Urusi wanadhibiti maeneo hayo.

Maafisa wa uchaguzi katika mji wa mashariki wa Donetsk wameiambia BBC kwamba hakuna vituo vya kupiga kura katika eneo hilo.

Mwandishi wa BBC anasema kuwa maafisa wa uchaguzi waliondoka katika kituo kimoja baada ya jengo la kituo hicho kufungwa.

Wagombea 18 wanawania wadhfa huo katika raundi ya kwanza ambayo inajiri wakati ambapo vikosi vya serikali vinakabiliana na wanamgambo wanaounga mkono Urusi mashariki mwa taifa hilo.

Iwapo hakuna mgombea atakayejipatia asilimia 50 ya kura hizo ,raundi ya pili ya uchaguzi huo itafanyika katika kipindi cha wiki mbili zijazo.

Mshindi atakabiliwa na jukumu kuu la kujaribu kuliunganisha taifa hilo mbali na kumaliza ghasia ambazo zimesababisha vifo vya watu 20 katika siku chache zilizopita.