Bendi yashambuliwa kwa msumeno Japan

Image caption Anna Iriyama mwanamuziki wa bendi aliyejeruhiwa Jumapili

Wanamuziki wawili wa bendi ya wanamuziki nchini Japan AKB48 wamejeruhiwa vibaya baada ya kushambuliwa na shabiki wao mmoja kwa kutumia msumeno.

Rina Kawaei mwenye umri wa miaka 19, na mwenzake Anna Iriyama 18, walikuwa wanakutana na mashabiki wao mjini Takizawa Jumapili wakati mwanamume mmoja alipowashambuliwa kwa msumeno.

Walipata majereha mikononi mwao na kwenye vichwa vyao. Mfanyakazi wao mmoja pia alijeruhiwa katika shambulizi hilo.

Kundi hilo linashikilia rekodi ya dunia kwa kuwa bendi kubwa zaidi ya wanamuziki duniani.

Polisi wamemkamata kijana mwenye umri wa miaka 24 kama mshukiwa wa shambulizi hilo.

Wasichana hao wawili walifanyiwa upasuaji na huenda wakaondoka hospitalini baadeye leo.

Image caption Rina Kawaei, alipata majeraha katika kidole chake

Tamasha walilokuwa wameandaa kufanyika Jumatatu , limefutilia mbali.

Bendi hiyo ni maarufu sana nchini Japan na katika mataifa mengine ya Asia.

Kadhalika kundi hilo lilianza kwa kuwa na wasanii 48 ingawa idadi hiyo imeongezeka hadi 140.

Kila mwaka mtu mmoja huteuliwa kujiunga na kundi hilo na pia wanachama hawaruhusiwi kuwa na ushirikiano wa kimapenzi.

Bendi hiyo iligonga vichwa vya habari mwaka jana wakati mmoja wa wasanii wake aliponyoa nywele zake zote kichwani na baadaye kuwoamba radhi mashabiki katika kanda ya video aliyoiweka kwenye mitandao ya kijamii.

Alikamatwa na wenzake akiwa na mpenzi wake.