Mikutano ya kisiasa yapigwa marufuku Kenya

Image caption Inspekta mkuu wa polisi David Kimaiyo

Serikali ya Kenya imepiga marufuku mikutano yote ya hadhara na kisiasa kwa muda usiojulikana katika mji mkuu Nairobi.

Inspekta mkuu wa polisi David Kimaiyo amesema kuwa sababu ya kuharamishwa mikutano ya hadhara ni kuwa magaidi wamepanga kufanya mashambulizi wakati wa mikutano yenyewe.

Akiongea baada ya mkutano wa maafisa wote wa ulinzi mjini Nairobi, Kimaiyo amesema kuwa hawataruhusu mikutano yoyote ya kisiasa wiki hii isipokuwa sherehe za kitaifa za kuadhimisha miaka hamsini na moja tangu kenya kujinyakulia utawala wa ndani kutoka kwa serikali ya Mkoloni.

Hizi zitakuwa sherehe za kusherehekea madaraka dei, zitakazofanyika tarehe mosi mwezi ujao.

Hata hivyo wakosoaji wa serikali wanasema kuwa uamuzi huo, unalenga mkutano wa upinzani uliopangwa kufanyika mwishoni wa wiki hii, kumlaki kiongozi wa muungano wa vyama vya upinzani CORD ambaye pia ni waziri mkuu wa zamani Raila Odinga ambaye amekuwa katika ziara ya miezi miwili nchini Marekani.

Naibu spika wa bunge wa zamani, na mwanasiasa wa upinzani Farah Maalim Mohamed amesema kuwa agizo hilo la inspekta mkuu wa polisi, halina msingi wowote na linakiuka katiba ya Kenya.

Marufuku hii inakuja siku chache kabla ya mkutano wa hadhara wa kisiasa uliopangwa na muungano wa upinzani wa CORD

Muungano huo umesema kuwa mkutano wao utafanyika kama ulivyopangwa, wakitaja marufuku hiyo kama ishara ya uoga kwa upande wa serikali.

Akihutubia wandishi wa habari baada ya kauli ya serikali kuharamisha mikutano, mmoja wa vigogo wa upinzani James Orengo, alisema kuwa marufuku hiyo ni njama ya serikali kuanzisha mfumo wa kidikteta sawa na uliokuwepo mapema miaka ya tisini.

Kiongozi mwingine wa upinzani Farah Maalim alisema kuwa watafanya mkutano wao wa kisiasa Jumamosi licha ya agizo hilo la serikali.