Maafisa wa Tume ya uchaguzi matatani Malawi

Image caption Shughuli ya kuhesabu kura Malawi imekumbwa na utata hasa katika maeneo ambako shughuli hiyo ilirejelewa

Mahakama kuu nchini Malawi imesema kuwa Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi na makamishna wa tume hiyo wanakabiliwa na mashitaka ya kudharau amri za mahakama.

Jaji Healey Potani wa mahakama kuu ya Blantyre amesema kuwa Jaji mwenzie Mack Mbendera na tume yake yote wamedharau mahakama kwa kuendelea na mipango ya kurudia kuhesabu kura ilhali Mahakama kuu kupitia kesi iliyowasilishwa na chama cha DPP iliiamuru tume hiyo kutangaza matokeo yote na kama kuna malalamiko yatafuata baadae.

Mwandishi wa BBC anayefuatilia uchaguzi huo, Baruan Muhuza ameripoti kuwa Jaji huyo alikuwa akitoa hukumu ya kesi iliyowasilishwa mahakamani hapo na mgombea urais Friday Jumbe wa chama cha New Labour kwa pamoja na wagombea binafsi kadhaa waliotaka tume hiyo kufuata sheria na amri iliyotolewa awali.

'Tume kufikishwa Kortini'

Image caption Wadadisi wameutaja uchaguzi wa Malawi kuwa kama Sarakasi

Mahakama hiyo sasa imetoa ruhusa ya kufunguliwa mashitaka dhidi ya Mbendera ambaye pia ni jaji wa Mahakama kuu nchini humo na wajumbe wote wa tume yake.

Hali hii inatazamiwa kuongeza utata katika suala zima la kupatikana hatma ya uchaguzi huo, ukizingatia kuwa Jumatatu usiku mwenyekiti wa tume hiyo aliwaambia waandishi wa habari kuwa, huenda mchakato huo ukachukua hadi siku 30 zijazo.

Hata hivyo Jaji Mbendera amesema tume yake inasubiri uamuzi wa Mahakama kuu ya Malawi iiongezee muda zaidi wa kuhesabu na kutoa matokeo, kwani muda wa sasa kisheria ni siku nane tu ambazo ni kama zimekwisha.

Wakati mivutano ikiendelea nao viongozi wa vyama mbalimbali nchini hapa wanawataka wafuasi wao na wananchi kwa ujumla kutulia na kusubiri tume ifanye kazi yake kwa mujibu wa sheria.