Wake wa Meya walio jela washinda uchaguzi

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Wapiga kura kwenye foleni

Wanawake wawili ambao waume zao ni wanasiasa wa upinzani waliofungwa jela nchini Venezuela, wameshinda uchaguzi wa Meya na kuchukua nafasi za waume wao ambao na wao walikuwa Meya kabla ya kufungwa jela.

Wanawake hao, Patricia Gutierrez na Rosa Brandonisio walishinda kwa asilimia 73 ya kura katika mji wa San Cristobal na asilimia 88 ya kura katika mji wa San Diego mtawalia.

Waume zao Daniel Ceballos na Vicencio Scarano waliokuwa Meya wa miji hiyo, walihukumiwa vifungo vya mwaka mmoja na miezi kumi mtawalia baada ya kupatikana na hatia ya kukosa kuondoa vizuizi ambavyo vilikuwa vimewekwa na wafuasi wao barabarani wakati wa maandamano.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Patricia Gutierrez akiwa na wanawe

Wanasiasa hao walifungwa jela mapema mwaka huu

Ushindi wa wanawake hao umepongezwa hata na baadhi ya wanasiasa kutoka chama tawala huku wakisema liwe funzo kwa wanasiasa wengine.

Venezuela imekuwa ikikumbwa na maandamano makubwa ya kupinga serikali tangu mwezi Februari.

Mazungumzo kati ya serikali na upinzani kusuluhisha mgogoro huo yamekwama kwa sasa.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Rosa Brandonisio (Katikati)

San Cristobal na San Diego ni ngome za upinzani na ushindi wa wanawake hao, sio jambo la kushangaza sana.

Lakini wadadisi wanasema ushindi wao utaimarisha upinzani dhidi ya chama tawala.

Miji hiyo miwili imeshuhudia vurugu mbaya zaidi ambapo watu 42 waliuawa kutoka pande zote mbili wa serikali na upinzani.

Maandamano yalianza baada ya wanafunzi kulalamikia kile walichosema ni ukosefu wa usalama.