Ghasia zaidi kupinga kombe la dunia

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Polisi mmoja alijeruhiwa kwa mshale

Polisi nchini Brazil wametumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji katika mji mkuu Brasilia wanaopinga kuandaliwa kwa kombe la dunia nchini humo.

Polisi walipigwa kwa mawe huku mamia ya waandamanaji wakijaribu kufika uwanja wa kitaifa ambako kombe litakalopokezwa washindi wa kinyang'anyiro hicho limewekwa.

Kikundi cha watu asilia wanaodai haki zao za kumiliki ardhi walijiunga na maandamano hayo

Haya ni maandamano ya hivi karibuni nchini Brazil kupinga gharama iliyotumiwa kuandaa kombe hilo.

Maafisa wakuu wanasema kuwa karibu watu 1,500 walihudhuria maandamano hayo yaliyofanyika Jumanne.

Waandamanaji hao walijaribu kwenda katika uwanja wa kitaifa ambao utakuwa mwenyeji wa mechi kadhaa za kombe la dunia ingawa polisi waliwazuia.

Polisi mmoja alijeruhiwa kwa mshale uliorushwa na mmoja wa waandamanaji wakati wa makabiliano kati ya polisi na waandamanaji hao.

Waandamanaji hao walitatiza pakubwa msongamano wa magari mjini Brasilia kwa masaa kadhaa.

Mwaka jana takriban watu milioni moja walishiriki maandamano kote nchini humo kutaka huduma bora zaidi za umma na kulalamikia ufisadi na gharama ya juu iliyotumiwa kuandaa kombe la dunia.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii