Al Shabaab wakiri kushambulia Djibouti

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Hali ilivyokuwa baada ya kushambuliwa kwa Bunge nchini Somalia

Al Shabaab wamesema katika taarifa kuwa kwa kushambulia mgahawa huo, walikuwa wakiwalenga raia wa mataifa ya Magharibi wanaopendelea kuutembelea Djibouti.

Kundi hilo liliwalaumu Wafaransa - walio na kambi kubwa ya wanajeshi nchini Djibouti - kwa kuwadhulumu Waislamu katika Jamhuri ya Africa ya Kati (CAR) na kwa kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Djibouti walio katika kikosi maalumu cha wanajeshi wa Umoja wa Afrika, AMISON, nchini Somalia.

Al Shabaab pia walilaumu Djibouti - ambayo ni mwenyeji wa vituo kadhaa vya kijeshi vya mataifa ya Magharibi, kukiwemo Marekani - kwa kuruhusu mataifa ya Magharibi kutumia taifa lao kama sehemu ya kushambulia Waislamu.

Al Shabaab wamepunguzwa makali nchini Somalia tangu kuanzishwa kwa msukumo wa kijeshi wa kukabiliana nao wa Serikali ya Somalia na wanajeshi wa AMISOM.

Hata hivyo kundi hilo halijaishiwa na uwezo wa kushambulia.

Mnamo Jumanne wanajeshi kadhaa wa Ethiopia waliuawa baada ya kuvamiwa na Al Shabaab katika eneo la Bakol.

Na Jumamosi, walishambulia Bunge katika mji mkuu wa Mogadishu.

Kwa kuwa kundi hilo tayari linaweza kushambulia nchini Kenya na sasa limechipukia Djibouti, ni ishara kamili kuwa limeanza kuwa tatizo katika eneo zima, mbali na kushambulia taasisi mbalimbali nchini Somalia.