Cameron azuru timu ya Kombe la Dunia

Haki miliki ya picha AP
Image caption Cameron aitembelea timu ya Kombe la dunia

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron ameitembelea timu ya taifa ya kombe la dunia katika kambi ya St George's Park iliyoko Burton na kufanya mazungumzo na kocha mkuu Roy Hodgson.

Cameron pia alipata fursa ya kutangamana na nahodha wa timu ya taifa Steve Gerrard na naibu wake Frank Lampard.

Ziara hiyo ya Cameron ilikuwa ya mwisho kabla timu hiyo haijachuana Peru na kuondoka kwelekea kwenye kipute hicho kitakachoanza tarehe 12 mwezi ujao huko Brazil.

Katika maandalizi ya kombe la dunia, beki wa timu ya taifa ya Luke Shaw huenda akakosa kushiriki mechi ya kirafiki dhidi ya Peru hii leo baada ya kushikwa na mafua.

Image caption Cameron aitembelea timu ya Kombe la dunia

Mkufunzi Hodgson amedhibitisha kwamba kikosi chake hakina matatizo ya majeraha ingawa Shaw anaugua.

Beki huyo mwenye umri wa miaka 18 aliichezea Uingereza mechi yake ya kwanza katika mchuano wa kirafiki dhidi ya Denmark mnamo mwezi Machi na kutajwa miongoni mwa wachezaji 23 watakaoshiriki kombe la dunia.

Tangu alipoanza kushiriki mechi za kimataifa, Shaw anadaiwa kuvutia vilabu kadhaa Uingereza, huku Manchester United ikidaiwa kutoa fedha za kutaka kumsajili.