Afrika Kusini yadorora kwa Hesabu na Sayansi

Haki miliki ya picha other
Image caption Afrika Kusini imeorodheshwa chini ya Kenya na Nigeria

Kuorodheshwa kwa Afrika kusini kama taifa linalofanya vibaya zaidi katika masomo ya hisabati na sayansi katika elimu duniani ni jambo la dharura linalopaswa kushughulikia haraka ipasavyo, upinzani umesema.

Chama cha The Democratic Alliance kimetaka uchunguzi wa ujuzi wa walimu wanaofunza hisabati, sayansi na teknolojia.

Ripoti iliyotolewa na kongamano la uchumi duniani (WEF) kuhusu teknolojia lilitathmini mataifa 148.

Serikali hata hivyo imepinga madai hayo, na kusema kuwa matokeo hayo yalitolewa kwa misingi ya mitazamo wala sio kwa uchunguzi kamili.

Ripoti ya kongamano hilo kuhusiana na teknolojia ya mawasiliano duniani hutathmini namna ambavyo mataifa yamejiandaa kutumia nafasi zinazotokana na mawasiliano na teknolojia ya mawasiliano na jinsi ambavyo yanaweza kuzitumia nafasi hizo kuimarisha hali yao.

Katika ubora wa elimu kwa ujumla, Afrika kusini iliorodheshwa ya 146 katika orodha iliyotolewa na WEF.

Ingawa sio mataifa yote yalitathmiwa, Afrika kusini iliorodheshwa chini ya Kenya, Nigeria na Zimbabwe.

'Kutisha'

Annette Lovemore, waziri wa elimu ya msingi alisema kuwa mwenzake wa serikalini Angie Motshekga anafaa kujibu maswali yote bungeni kuhusu 'kudorora' kwa kwa elimu nchini humo.

Haki miliki ya picha AP

Shirika la Afrika Kusini la Eyewitness linamnukuu Bi Lovemore akisema kuwa ni jambo la kukera sana, sio tu kwa kuwaangusha mamia ya maelfu ya wanafunzi shuleni bali pia kuangusha uchumi wao unaostahili ujuzi utokanao na hesabu na sayansi.

Bi Motshekga anayehudumu katika idara ya elimu ya msingi alifutilia mbali ripoti hiyo na kusema kuwa ''ilifanywa kutokana na mahojiano uliofanywa na watendaji wa sekta ya biashara.

Hata hivyo, bi Lovemore alisema kuwa hakukuwepo na ‘upenyaji wa uongo’ katika ripoti hiyo- ijapokuwa palikuwepo na kuboreka kwa miaka ya hivi karibuni, ‘jambo zima bado ni la kuogofya.’

Alisema kuwa asilimia 90 ya wanafunzi wenye umri wa miaka 15 walishindwa kufikia ‘kiwango kidogo cha mafanikio’ katika hesabu na sayansi katika utafiti uliofanywa mwaka wa 2003 duniani.

Tarakimu hii ilipungua hadi asilimia 76 mwaka wa 2011.

Mtangazaji wa BBC Pumza Fihlani aliye mjini Johannesburg anasema kuwa mwaka uliopita jopo maalum la wizara lilichunguza jinsi ambavyo masomo ya hesabu, sayansi na teknolojia inavyofunzwa na likapata hatari inayokumba mfumo wa elimu wa taifa hilo.

Shule zilizoathirika pakubwa zaidi ni zile zilizo mashambani, ambako hakuna vifaa vya kufunzia na pia walimu kukosa kuhudhuria masomo.