UN-'Pande zote CAR zilihusika na uhalifu'

Haki miliki ya picha
Image caption Vurugu CAR

Ripoti ya umoja wa mataifa inasema kuna ushahidi wa kutosha kuwa pande zote mbili zinazozozana katika mgogoro wa kisiasa katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati, zimehusika katika uhalifu wa kivita na vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu.

Hata hivyo umoja wa mataifa katika ripoti hiyo inasema kuwa bado ni mapema kusema kuwa mauaji ambayo yametokea nchini humo ni ya kimbari ama ya kikabila.

Mapema mwezi Februari mwaka huu shirika la kimataifa la Amnesty International liliuelezea mgogoro wa kivita na machafuko nchini humo na mapigano yanayoendelea wa kikabila na kuyashutumu mashirika ya kimataifa kuchelewa kupata ufumbuzi.

Mwaka jana Jamhuri ya Afrika ya Kati imejikuta katika mgogoro wa kidini pale kundi la wapiganaji wa kiislam la Seleka lilipoanzisha mapigano katika nchi ambayo idadi kubwa ni waumini wa dini ya kikristu.

"Ni ushahidi wa wazi kwamba pande hizo mbili walivunja haki za kimataifa za binadamu kwa kutenda makosa ya mauji pamoja na kushiriki vita’’imesema ripoti hiyo.

Jumuiya za kimataifa pia zimetahadharishwa na ripoti hiyo kuwa makini na mgogoro huo wa Afrika ya kati na kutopeleka kwa haraka vikosi vya askari wa kulinda Amani nchini humo kwa madai kuwa hatua hizo zinaweza kusababisha kutokea kwa mauaji ya kimbari na kuhamasisha mgawanyiko wa kikabila.