Rais mpya wa Ukraine kuapishwa

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Poroshenko alikutana kwa mara ya kwanza na Rais wa Urusi Vladimir Putin Alhamisi

Rais mteule wa Ukraine Petro Poroshenko amepongeza mkutano wake na rais wa Urusi Vladmir Putin kama mwanzo wa majadiliano kuhusu mzozo unaondelea mashariki mwa Ukraine.

Bwana Poroshenko ambaye anatarajiwa kuapishwa rasmi kama kiongozi wa taifa hilo hilo amesema kuwa mazungumzo mengine na Urusi yatafanyika hapo kesho siku ya Jumapili.

Bwana Putin amesema kuwa vita vinafaa kusitishwa katika eneo hilo kabla ya majadiliano kuanza.

Vilevile amemuonya bwana Poroshenko kwamba iwapo Ukraine itaingia katika mkataba wa kibiashara na muungano wa Ulaya,Urusi itachukua hatua za kuutetea uchumi wake.

Viongozi hao wawili walikutana pembezoni mwa siku ya kusherehekea wakongwe wa vita mjini Normandy nchini Ufaransa.

Ni mkutano wa kwanza tangu kuchaguliwa kwa bwana Poroshenko mnamo mwezi Mei.

Kiev inatuhumu Moscow kwa kuunga mkono wapiganaji wa maeneo ya kusini mwa nchi wanaotaka kujitenga,madai ambayo Kremlin imekanusha.

Mapigano yaliendelea Ijumaa huku waasi wanaounga mkono Urusi, wakiripotiwa kudungua ndege ya serikali karibu na eneo linalodibitiwa na waasi la Sloviansk.

Msemaji wa jeshi la Ukraine aliambia vyombo vya habari kwamba ndege hiyo ilikuwa inabeba chakula cha msaada , lakini taarifa hizi hazijaweza kuthibitihshwa.

Awali wanajeshi wa serikali walifanya mashambulizi karibu na mji huo.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii