Jeshi la Nigeria lavamia magazeti

Haki miliki ya picha AP
Image caption kampuni ya gazeti nchini Nigeria

Jeshi la Nigeria limevamia vituo vya kusambaza magazeti.

Gazeti la daily Trust linalonunuliwa na raia wengi wa taifa hilo limesema kuwa jeshi liliwakamata madereva wake pamoja na magari ya kusambaza magazeti siku ya Ijumaa na Jumamosi katika maeneo mbalimbali nchini humo.

Magazeti yaliotoa ushahidi kama huo ni The Punch,Leadership pamoja na gazeti la Nation.

Msemaji wa wizara ya Ulinzi nchini Nigeria Meja jenerali Chris Oluko-lade amesema kuwa vitendo vya wanajeshi hao ni miongoni mwa oparesheni za kila mara za kiusalama.

Jenerali huyo amekana madai kwamba baadhi ya nakala za magazeti zilichukuliwa.

Chama cha wahariri nchini humo kimefananisha hatua hiyo na udhibiti wa matangazo wakati taifa hilo lilipokuwa likiendeshwa kijeshi.

Jeshi nchini humo limekosolewa na vyombo vya habari kuhusiana na vile linavyoliangazia swala la wanamgambo wa Boko Haram pamoja na madai kwamba maafisa wakuu wa jeshi wamekuwa wakiwasaidia kisiri wanamgambo hao.