ICC:Tuna ushahidi dhidi ya Ntaganda

Haki miliki ya picha .
Image caption Ntaganda akiwa katika mahakama ya ICC

Mahakama ya kimataifa ya Uhalifu wa kivita,ICC imesema kuwa imepata ushahidi wa kutosha kumfungulia mashitaka mbabe wa kivita wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo Bosco Ntaganda.

Ntaganda anashutumiwa kwa makosa ya Ubakaji, mauaji na hata kuwasajili watoto wadogo kama wapiganaji wakati wa vita vya mashariki mwa DRC.

Bosco Ntaganda, anayefahamika kwa umaarufu zaidi kama Terminator, anakabiliwa sasa na mashitaka kumi na nane ya uhalifu wa kivita, mauaji na pia kuwafanya watu watumwa katika vita.

Mahakama hiyo ilipokea ushahidi wa zaidi ya nyaraka elfu sitini na tisa kwa hivyo mwendesha mashtaka ameezelea imani kuwa anayo kesi ya kutosha kumfungisha Ntaganda.

Mnamo mwezi Machi mwaka huu, Bwana Ntaganda alijisalimisha mwenyewe kwa ubalizo wa Marekani Mjini Kigali ambao ulimpokea na kumkabidhi kwa mahakama ya ICC mjini The Hague.

Licha ya kuwa wanadai kupata ushahidi wa kutosha, Mahakama hiyo sasa itakabiliwa na kibarua kigumu kubainisha kuhusika moja kwa moja kwa bwana Ntaganda katika makosa wanayomshitaki nayo.

Mawakili wanasema kuwa mauaji ya Uvira, mashariki mwa DRC yalilenga makabila ya Lendu, Bira na Nande.

Shirika la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch limesema kuwa hatua ya kumfungulia mashitaka Bosco Ntaganda ni hatua muhimu katika kuwalipizia haki waathiriwa wa mauaji ya DRC.

Wamesema pia kuwa huu ni ujumbe kwa wababe wa kivita kuwa hatimaye watakabiliwa na sheria kwa uhalifu dhidi ya binadamu.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii