Kero za wakulima Tanzania

Image caption Wakulima Tanzania

Tanzania ina eneo kubwa ambalo linafaa kwa shughuli za ukulima ikilinganishwa na nchi nyengine za Afrika Mashariki.

Lakini ni nusu tu ya eneo hilo ambalo linatumika kwa ukulima, na idadi kubwa ya wakulima bado wanatumia mbinu za kizamani.

Takwimu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika zinaonyesha kwamba robo tatu ya watanzania wapatao milioni arobaini na sita ni wakulima wadogo wadogo, wengi wao wakiwa ni wanawake.

Wengi wa wakulima hao wanasema kipato wanachopata sio kikubwa,ingawa kinaweza kuwalipia watoto karo ya shule, kujenga nyumba ya wastani na hata kulisha familia. Wao sio matajiri.

Image caption Baadhi ya wakulima wamelalamikia ukosefu wa soko la uhakika

Kesiah Abele ni mkulima mdogo katika kijiji cha Valesca, nje ya mji wa Arusha, ambaye analalamikia miundo mbinu mibaya ya barabara kuwa ndio inayochangia kipato chake kutoongezeka.

"Kwa sababu hatuna miundo mbinu mizuri ya barabara, hivyo inabidi tuuze mazao yetu kwa bei ya chini hivyo hivyo. Masoko yako mbali na kijiji chetu, na kwa sababu hiyo mazao yetu hayapati bei nzuri. Lakini hatuna la kufanya," Kesiah amesema.

'Biashara duni kwa wakulima'

Uhusiano wa wachuuzi na wakulima mara nyingi huo sio mzuri kwa sababu wanunuzi hupenda kuwalalia wakulima katika bei kwa kisingizio kwamba wao pia hutumia muda mwingi na fedha nyingi kufika mashambani kwa ajili ya kununua bidhaa.

Hii sio mara ya kwanza kwa wakulima kuzungumzia kero zao na wengine wanahisi kwamba hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa kwa ajili ya kutatua kero hizo.

Image caption Miundo mbinu duni ya barabara inatajwa kuchangia kipato cha chini cha mazao

Hata hivyo, ni matumaini yao hivi sasa kwamba baada ya matatizo yao kuainishwa katika utafiti uliofanywa na Redio ya Wakulima ya Kimataifa, hivyo viongozi mbali mbali wataweza kuchukua hatua.

Gerson Shao ambaye pia ni mkulima mdogo kutoka kijiji cha Kwita pembezoni mwa Mlima Kilimanjaro, amemwambia mwandishi wa BBC Aboubakar Famau kwamba anatumai majibu ya kura zilizofanywa na wakulima yatafanyiwa kazi ili kuleta mabadiliko.

Baadhi ya wakulima hawa, wamekuwa katika wakifanya shughuli za ukulima kwa takriban miongo kadhaa sasa, huku wengine wakiwa wamerithi ujuzi huo kutoka kwa wazazi wao.

Lakini jinsi inavyokuwa taabu kupata faida kutokana na ukulima, huenda vizazi vijavyo vikaibeza sekta hiyo ambayo ina uwezo mkubwa wa kuinua maisha ya watu.