Vita vya kikabila vyatokota Somalia

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Somalia inakumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe

Takriban watu 7 wameuawa nchini Somalia katika vita vya kikabila mkoa wa Galgaduud, katikati mwa Somalia.

Hii inakuja wakati kuna vita vingine vya kikabila kule Marka, kilomita 90, kusini mwa mji mkuu Mogadishu.

Miezi miwili baada ya wanajeshi wa muungano wa Afrika kudhibiti takriban miji kumi katikati na kusini mwa Somalia, vita vya kikabila vimemeanza kuzuka katika baadhi ya maeneo yanayosimamiwa na serikali ya Somalia.

Kabila mbali mbali zimeanza kuzozania utawala wa maeneo hayo.

Serikali ya Somalia, imeagiza pande zinazopigana kusitisha vita na kumaliza tafauti kati yao kwa kuzungumza.

Mkuu wa mkoa wa Galgaduud, ameiambia Idhaa ya Kisomali ya BBC kuwa, wanajaribu kusuluhisha tofauti kati ya jamii tafauti, ingawa hawana uwezo wa kijeshi. Amesema wanajeshi wao wanasimamia miji na siyo vijijini ambako vita vimezuka.

Wadadisi wanasema, vita vya kikabila havikushuhudiwa kwa maeneo haya wakati kundi la Al-Shabaab lilikuwa likilidhibiti

Wanasema mapigano yamerudi tu baada ya Al-Shabaab kuondolewa kutoka maeneo haya.

Hata hivyo, maafisaa wa serikali ya Somalia, wanalaumu kundi la Al-Shabaab kwa kuchochea vita vya kikabila kwa maeneo haya.