Je Urembo wa kujichubua ni urembo?

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Picha za hivi karibuni za Vera Sidika kwenye mitandao ya kijamii

Swala la kubadili rangi ya ngozi limekuwa kama msumari moto, kunao wanaoliunga mkono na wale wanaolipinga swala hilo katu hawawezi kulifanya.

Baadhi wanasema kuwa ni wanawake wasiojithamini na kujiamini pekee ndio wenye kujichubua ngozi.

Mjadala huo ukiendelea, wasichana wengi wanajitafutia umaarufu sio Marekani na Uingereza tu bali hata katika kanda ya Afrika ya Mashariki. Wasichana hao wamekuwa wakifanya kila wawezalo ili kupata huo umaarufu.

Mmoja wa wasichana hao ni Vera Sidika anayejulikana sana nchini Kenya na Afrika mashariki kwa kuwa na makalio makubwa ambayo ndiyo yaliyompa umaarufu wake baada ya kuonekana katika wimbo mmoja wa video uitwao 'You Guy' ambao baadaye ulipigwa marufuku nchini Kenya.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Picha za awali kabla ya Vera kujichubua ngozi

Vera amejizidishia umaarufu kwa kubadili rangi yake ya ngozi, zamani kidogo akiwa mweusi na sasa amejichubua na kuwa mweupe na pia kuwaambia watu kuwa kubadili rangi ya ngozi yake ni yeye mwenyewe kujitakia. Hiyo isiwashughulishe watu.

Vera anajulikana kwa kuwa na mazoea ya kujipiga picha hasa za makalio yake na kuziweka kwenye mitandao ya kijamii. Vara analinganishwa sana na Kim Kardhashian hasa kwa sababu ya umbo lake.

Kazi ya Vera hasa ni ya uwanamitido lakini mbali na hilo Vera hulipwa ili kufika kwenye karamu mbali mbali , kwenye disco na katika hafla mbali mbali za watu mashuhuri. Yeye pia hulipwa kuwa katika kanda za video za wanamuziki maarufu Afrika Mashariki.

Alifichua kupitia televisheni Ijumaa kuwa alitumia maelfu ya dola kubadili rangi ya ngozi yake na kujifanya mweupe.

Shughuli hiyo aliifanyia nchini Uingereza na ilimgharimu karibu milioni 15 pesa za Kenya, hizo ni dola 170,000 na kwamba tayari kuna watu wengi wanaotaka sana kujichubua ngozi na kufanana na Vera, kwa mujibu wa mwanadada huyo.

Image caption Vera ni mwanamitindo na anapanga kufungua duka la kuuzwa bidhaa za urembo

Vera anasema kuwa watu wamemsema sana kwenye mitandao ya kijamii vibaya kwa sababu ya anavyoendesha maisha yake. Amewataja kama wanafiki kwa sababu anasema huku wakiendelea kumsema na kumkosoa kwa kujichubua, wamekuwa wakimuuliza alichofanya ili na wao watafute pesa wakafanye hivyo kwa wanataka sana kufanan naye.

Mtindo wa wanawake kujichubua ni swala tata nchini Kenya. Sio kama India ambako vipodozi vya kujichubua huuzwa wazi wazi. Nchini Kenya bidhaa hizo, huuzwa kimagendo.

Wataalamu wanasema, wanawake wengi wanaendelea kujichubua licha ya hatari za bidhaa zinazouzwa kimagendo.

Swala la wanawake kijichubua barani Afrika lilianza kujadiliwa waziwazi pale ambapo msanii raia wa Cameroon Dencia kuzindua rasmi bidhaa zake za kuchubua ngozi ziitwazo, Whitenicious.