Wanajeshi wa Iraq waimarisha doria

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Wapiganaji wa kundi la JIhad la ISIS

Wanajeshi watiifu wa serikali ya Iraq wameimarisha doria katika mji wa Samarra dhidi ya wanamgambo wa kundi la Jihadi ISIS ambao wanadhibiti eneo kubwa la Magharibi na Mashariki mwa taifa hilo.

Vikosi vya serikali vimeungana na wanamgambo wanaounga mkono Serikali kufuatia ombi la waziri mkuu Nouri Al Malik na kiongozi wa dhehebu la Shia nchini humo Ayatollah Ali al Sistani.

Bwana Malik amedaiwa kuzuru mjini Samarra ambapo upo zaidi ya kilomita mia moja kutoka mji mkuu wa Baghdad.

Jenerali mmoja wa Iran anadaiwa kuwa mjini Baghdad licha ya Iran kukana madai kwamba vikosi vyake vimeingia nchini Iraq.

Rais Obama ameonya kutekeleza mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya wanamgambo hao ambao amesema kuwa si tishio tu kwa Iraq na raia wake bali pia maslahi ya Marekani.

Wakati huohuo serikali ya Iraq imeripotiwa kuifunga mitandao ya kijmii nchini humo kwa hofu kwamba huenda inatumiwa na wanamgambo wa Isis ili kuwaajiri wanachama zaidi mbali na kueneza vitisho.

Kundi la Isis pia limeshtumiwa kwa kutekeleza uhalifu wa kivita katika miji ilioteka.

Kundi hilo limetoa onyo kwamba watu zaidi watauawa iwapo watakataa kuheshimu sheria wanazoweka.