Jumuia yatoa ripoti kuhusu DRC na Rwanda

Image caption Mpaka wa mataifa ya Maziwa Makuu kukiwemo DRC na Rwanda.

Wachunguzi kutoka jumuiya ya mataifa ya eneo la maziwa makuu wamechapisha ripoti kuhusu mapigano ya hivi karibuni yaliyotokea katika eneo la mpaka kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda.

Ripoti hiyo inasema kuwa mapigano hayo yalitokana mzozo wa ardhi kati ya mataifa hayo mawili katika maeneo ya milima miwili jirani. Mwandishi wetu wa Kinshasa Lubunga Byaombe ameisoma ripoti hiyo na kutuandalia taarifa ifuatayo.

Kulingana na mwandishi wetu wa Kinshasa, Lubunga Byaombe, wanachama wa tume hiyo walitembelea pande zote mbili za mpaka na kuthibitisha kuwa Rwanda ilikuwa ya kwanza kulalamika kufuatia habari za wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo walivuka na kuingia nchini Rwanda kwa lengo la kutaka kuiba ngombe.

Ripoti hiyo inasema kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa upande wake inasema kuwa Rwanda mara kwa mara haiheshimu mpaka ulio kati ya mataifa hayo mawili na wanajeshi wake huvuka mara kwa mara na kuingia katika taifa lake.

Hata hivyo ripoti hiyo inasema kuwa mapigano ya hivi majuzi yanatokana na kutokuwepo mpaka kamili kati ya mataifa hayo mawili.

Katika mapigano hayo ya hivi karibuni mataifa hayo yalikuwa yakizozania milima miwili ambayo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilidai yote ni yake huku Rwanda ikisema inamiliki mlima mmoja.