Marekani yashinikiza amani Iraq

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption John Kerry na waziri mkuu Nouri al Malik

Waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani John Kerry amewasili nchini Iraq na kuonya kuwa Iraq inakabiliwa na wakati mgumu katika historia yake.

Kerry amewasihi viongozi wa kisiasa nchini humo kubuni serikali ya umoja ili kuepuka mgawanyiko wa kidini.

Wapiganaji wa ki-suni likiwemo kundi lenye itikadi kali la Isis wameiteka miji minne zaidi mkoani Anbar magharibi mwa Baghdad na kuviteka vivukio viwili vya mpakani katika barabara inayoelekea Syria.

Usalama umeimarishwa Kaskazini mwa Baghdad eneo ambalo lina wakaazi wengi wa raia wa ki-sunni.

Watu wa Dhehebu la Sunni ni wachache nchini Iraq na hawaipendi serikali ya waziri Mkuu Nouri al Malik kwa kuwa inatawaliwa na watu wengi wa dhehebu la Shia.

Wakati huohuo imethibitishwa kwamba wapiganaji wa ki-sunni nchini Iraq wameuteka mji wa Tal Afar unaomiliki uwanja wa ndege wa kijeshi.

Mji huo ndio unaomiliki barabara kuu inayotoka katika mpaka wa Syria hadi mji wa Mosul,ambao ndio mji wa pili kwa ukubwa nchini Iraq.

Habari kuhusu kutekwa kwa mji wa Tal Afar zinajiri baada ya wanamgambo kuuthibiti maeneo yote ya mpakani ya mkoa wa magharibi wa Anbar.

Mwandishi wa BBC anasema kuwa kutekwa kwa Tal Afar ni pigo kwa serikali ya Iraq iliopanga kuutumia mji huo kuuteka mji wa Mosul.