Marufuku ya Miraa yaanza kutekelezwa

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Ni kilio nchini Kenya wakulima wakohofia kupoteza ajira

Marufuku ya utafunaji wa miraa nchni Uingereza inaanza kutekelezwa leo, nchini Uingereza. Mmea huo hutafunwa na watu wengi wenye asili ya kisomali , Yemen na Ethiopia,

Serikali ya Uingereza inasema kuwa kuharamishwa kwa Miraa nchini Uingereza inaambatana na hatua zilizochukuliwa na mataifa mengine ya Ulaya pamoja na Marekani ambako Miraa ni haramu.

Watumiaji wa mmea huo wanasisitiza kuwa sio hatari kuutumia na kwamba kuupiga marufuku ni ubaguzi dhidi ya jamii ambazo ni za wachache.

Mmoja wa watu ambao wamekuwa wakiutumia mmea huo, Aden Haj anasema alitelekezwa na familia yake ambayo haingeweza kustahamili utumiaji wake wa Miraa na anawataka watu kufahamu athari za kutumia Miraa.

Image caption Majani ya Miraa ambayo Uingereza inasema ni sawa na dawa za kulevya

Nchini Kenya ambako mmea huo unakuzwa, maelfu ya wakulima katika eneo la Meru sasa wanakabiliwa na tishio la kupoteza mamilioni ya pesa baada ya marufuku ya kusafirisha miraa nchini Uingereza kuanza kutekelezwa.

Hatua hiyo inajiri baada ya Uingereza kuharamisha utafunaji wa miraa nchini humo baada ya mmea huo kuorodheshwa miongoni mwa madawa ya kulevya.

Uingereza ni mojawepo wa mataifa ya bara Ulaya yaliyokuwa yakitoa soko kubwa zaidi kwa zao la miraa kutoka Kenya kutokana na idadi kubwa ya watu wa jamii ya wasomali wanaoishi nchini humo.