Helikopta yadunguliwa na kuua 9 Ukraine

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Helikopta sawa na ile iliyodunguliwa Ukraine na kuwaua watu 9.

Maafisa wa wizara ya ulinzi nchini Ukraine wamesema kuwa waasi wanaotaka kujitenga ambao wanaiunga mkono Urusi wamelipua ndege iliyokuwa imewabeba wanajeshi wa serikali na kuwauwa watu tisa.

Shambulio hilo lilifanywa karibu na mji wa Sloviansk unaodhibitiwa na waasi mashariki mwa taifa hilo.

Kulingana na maafisa wa Ukraine, helikopta hiyo ilipigwa risasi nje ya makao makuu ya Sloviansk.

Wanajeshi saba wa Ukraine ni miongoni mwa watu waliofariki katika tukio hilo.

Kudunguliwa kwa helikopta hiyo kumetokea muda mufpi baada ya Serikali na upande wa kundi linalotaka kujitenga kutoka kwa Ukraine linaloungwa mkono na Urusi kutangaza usitishaji wa mapigano.

Mnamo Jumanne Rais wa Urusi, Vladimir Putin, alitoa wito kwa Wabunge kubadilisha upigaji kura walioufanya Machi, uliomruhusu yeye kuwa na mamlaka ya kuingilia kijeshi maswala ya Ukraine.

Serikali ya Ukraine na mataifa ya Magharibi wanasema kuwa Urusi inawaruhusu wapiganaji na silaha kuingia Ukraine, hatua ambayo inachochea uasi unaoendelea nchini humo.

Lakini kiongozi wa eneo linalopiganiwa wakati huu linalotaka kujitenga lililojitangaza kama "jamhuri ya watu wa Donetsk", Alexander Borodai amesema kuwa kwa maoni yake haoni maana yo yote ya kusitisha mapigano.

"Nasema rasmi sasa kuwa hakujakuwepo na usitishaji mapigano na ukichunguza kwa makini kinachoendelea hakutakuwepo na usitishaji huo wa mapigano....kwa ujumla, kilichosalia kwetu sisi ni kuendelea kupigana," Alexander Borodai alisema.

Wakati huohuo Rais wa Urusi, Vladmir Putin, amesema kuwa haitoshi kwa Ukraine kutangaza siku saba za usitishwaji wa mapigano kati yake na waasi Mashariki mwa Ukraine.

Alisema mashauriano mengine kambambe yanapaswa kuandaliwa ili kuwahakikishia wachache wanaozungumza lugha ya Kirusi wanaoishi nchini Ukraine haki zao za kimsingi.