Bomu:Rais wa Nigeria aahirisha ziara

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais wa Nigeria Goodluck Johnathan

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan ameahirisha ziara yake nchini Equitorial Guinea kufuatia shambulizi la bomu la siku ya Jumatano katika mji mkuu wa Abuja,kulingana na msemaji wake.

Usalama umeimarishwa katika mji huo kufuatia shambulizi hilo lililowauwa watu 21 na kuwajeruhi wengine 52.

Hatua ya Bwana Johnathan kurudi inafuatia shtuma kwamba ameshindwa kukabiliana na ghasia nchini humo.

Wapiganaji wa kundi la Boko haram wameimarisha mashambulizi yao nchini Nigeria.

Mnamo mwezi Aprili,wapiganaji hao waliwauwa zaidi ya watu 70 katika mlupuko wa bomu katika kituo kimoja cha basi viungani mwa mji wa Abuja.

Kundi hilo pia limekiri kutekeleza shambulizi la bomu lililotegwa ndani ya gari karibu na kituo cha mabasi katika kijiji cha Nyanya mnamo mwezi May,ambalo liliwauwa watu 19 na kuwajeruhi wengine 60.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption kiongozi wa Boko Haram Abubakr Shekau

Hatahivyo kundi hilo halijatoa tamko lolote kuhusu mlipuko wa hivi karibuni.

Maafisa wa Polisi wanasema kuwa mshukiwa mmoja amekamatwa lakini hawajatoa maelezo yoyote kumhusu.

Msemaji wa rais Reuben Abati amesema kuwa Jonathan alipata habari kuhusu mlipuko huo wakati alipokuwa akiwasili katika hoteli yake katika mji wa Malabo nchini Equitorial Guinea alikoelekea kwa mkutano umoja wa afrika kulingana na gazeti la Premium Times nchini Nigeria.

Aliamua kurudi nchini Nigeria ili kukabiliana na tatizo hilo,alisema bwana Abati.

Mwandishi wa BBC Mansur Liman katika mji wa Abuja anasema kuwa vikosi vya usalama vimelitenga eneo hilo la mlipuko.

Maafisa wa polisi wameagiza kuongezwa kwa usalama pamoja na uchunguzi ndani na hata viungani mwa mji wa Abuja ili kuepuka mashambulizi zaidi,alisema.