NACADA yaharamisha ladha za Shisha

Image caption Ladha kadhaa za Shisha kpigwa marufuku kwa hofu kuwa zinachanganywa na dawa za kulevya

Shirika la kupambana na madawa ya kulevya nchini Kenya, NACADA, limeharamisha ladha kumi na tisa za Shisha.

Kwa mujibu wa afisaa mkuu mtendaji wa shirika hilo Fazul Mohammed, shirika hilo kwa ushirikiano na wanasayansi wa serikali waligundua kuwa ladha hizo wakati mwingi zinakuwa zimechanganywa na madawa ya kulevya kama vile Cocaine na Heroine.

Utafiti wao waliufanya kisiri katika mikahawa maarufu yenye kuuza Shisha na hapo ndipo waligundua kuwa nyingi ya ladha za Shisha huwa zimechanganywa na madawa ya kulevya.

Baadhi ya ladha hizo pia ziligunduliwa kuwa na Bhangi.

Image caption Mwenyekiti wa shirika la kupambana na dawa za kulevya Kenya, John Mututho

Akiongea na BBC bwana Fazul alisema kuwa shirika hilo linatafakari kupiga marufuku Shisha kwa sababu ya madhara yake kwa afya ya watumiaji na hasa kwa kuwa nyingi zinachanganywa na madawa ya kulevya.

Ladha hizo ambazo zinapaswa kuondoshwa sokoni mara moja ni pamoja na Al Fakher yenye ladha ya strawberry , Al Fakher yenye ladha ya chungwa , Al Fakher yenye ladha ya tufaha, Al Fakher vanilla , Al Fakher Mapera, Al Fakher appeals, Al Fakhar chungwa ikiwa na ladha ya mint na nyinginezo.

Kwa mujibu wa Bwana Fazul , kwa wale watakoapatikana wakitumia Shisha lenye ladha hizo ambazo zimepigwa marufuku, watashitakiwa.

Mwenyekiti wa tume ya shirika hilo, John Mututho, amenukuliwa akisema watakaopatikana wakiuza au kutumia bidhaa hizo, watafikishwa mahakamani.