Pistorius:Daktari apata mshtuko wa moyo

Haki miliki ya picha
Image caption Mwanariadha Pistorius akiwa mahakamani

Daktari wa akili anayetathmini hali ya mwanariadha Oscar Pistorius katika kesi ya mauaji ya mpenziwe Reeva Steenkamp amepatwa na mshtuko wa moyo.

Hatahivyo swala hilo halitarajiwi kucheleweshwa kusikizwa kwa kesi hiyo ambayo itaendelea siku ya jumatatu,upande wa mashtaka umesema.

Bwana Pistorius anatarajiwa kukamilisha siku thelathini za utathmini wa akili yake.

Jaji katika kesi hiyo aliagiza kufanywa kwa ukaguzi huo baada ya shahidi mmoja wa Pistorius kusema kuwa mshtakiwa huyo alikuwa anakabiliwa na ugonjwa wa wasiwasi.

Mwanariadha huyo amekana kumuua mpenziwe kimakusudi na anasema kuwa alimpiga risasi kwa bahati mbaya kupitia mlango wa choo siku ya Valentine mwaka uliopita alipodhani kwamba mwanamke huyo wa miaka 29 alikuwa ni jambazi.