Uchina haitatumia mabavu kwa wengine

Haki miliki ya picha AP
Image caption Rais Xi Jinping amesema nchi yake haitawahi kutumia nguvu dhidi ya mataifa mengine

Rais Xi Jinping wa Uchina amesema nchi yake daima haitojaribu kulazimisha nchi nyengine kufuata matakwa ya Uchina, hata Uchina itapokuwa na nguvu kubwa zaidi.

Alisema hayo mjini Beijing ambapo aliwapokea viongozi wa India na Myanmar (Burma).

Rais Xi alisema tabia ya uonevu na kutumia nguvu za kijeshi haimo katika damu ya watu wa Uchina, na kwamba enzi za mabavu ya mataifa makuu zimekwisha.

Mwandishi wa BBC mjini Beijing anasema hotuba ya Rais Xi ilikusudiwa kuwatuliza majirani wa Uchina pamoja na Marekani, ambao wana wasi-wasi kwa vile bajeti ya jeshi la Uchina inazidi kuongezeka, na kile kinachoonekana kama sera ya Uchina ya kudai ardhi katika mizozo kadha na majirani zake.

Mkutano unaofanywa Beijing unaadhimisha miaka 60 ya makubaliano ya ushirikiano wa salama uliotiwa saini na Uchina, India na Burma - ambayo piya inajulikana kama Myanmar.

Na nchini Taiwan shughuli mbili zimefutwa wakati wa ziara ya afisa mwandamizi wa Uchina, baada ya waandamanaji kuurushia rangi msafara wa magari yaliyokuwa yakimsindikiza afisa huyo.

Zhang Zhijun, ambaye amemaliza ziara ya siku nne Jumamosi, hakuumia katika mvurugano huo.

Watu wengi wa Taiwan hawapendi Uchina kuonesha madaraka yake juu ya kisiwa hicho kinachojitawala, na ambacho Uchina inakiona kama ni chake.

Katika miaka ya karibuni kiongozi wa Taiwan amekuwa akijaribu kuzidisha fungamanisho za kibiashara baina ya nchi mbili hizo.

Siku ya Ijumaa, Bwana Zhang alisema Beijing inaheshimu uamuzi wa watu wa Taiwan kuhusu aina ya maisha yao na mfumo wao wa jamii.