Mama amtelekeza mtoto ndani ya karatasi

Mwanamke mmoja aliyemtelekeza mwanawe ndani ya karatasi ya plastiki katika bustani moja nchini Uingereza aponea adhabu ya kifungo jela.

Mtoto huyo mchanga aliyekuwa wa siku moja tu, alipatwa na mtu aliyekuwa anamtembeza Mbwa wake katika bustani hilo.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 27, alihukumiwa kifungo cha nje cha miezi sita na kuwekwa chini ya ulinzi wa maafisa wa kijamii kwa miaka miwili.

Hata hivyo alikiri kumtelekeza mtoto wake kwa maksudi na kusema kuwa aliathirika kimawazo baada ya kujifungua mtoto huyo mwezi Mei.

Polisi walisema kuwa mtoto huyo alinusurika kifo kwa dakika thelathini tangu kutelekezwa kwani alipatikana haraka sana na kwamba mwili wake tayari ilikuwa umeanza kuwa baridi.

Mtoto huyo alipatikana mwaka jana akiwa amefungwa ndani ya taulo na kuwekwa ndani ya karatasi ya Plastiki katika bustani hilo.

Mama huyo aliambia mahakama kuwa alifanya kitendo chake katika hali ya kutojielewa.

Pia alifahamisha mahakama kuwa alijifungulia mtoto wake katika sakafu ya bafu nyumbani kwa mamake hali ambayo ilimuathiri kimawazo.

Alificha ujauzito wake kutoka kwa familia yake na pia hakuwahusisha madaktari kwa sababu alihofia kuwa hangeweza kustahamili ujauzito wake.

Mahakama pia ilifahamishwa kuwa mwanamke huyo ana watoto wengine ila ameachana na baba yao.

Jaji alisema kuwa mtuhumiwa anakumbwa na shinikizo la mawazo hasa baada ya kujifungua mtoto wake. Mumewe alipoachana naye, hali yake ikaanza kuzorota zaidi hali ambayo ilisababisha mahakama kutompa adhabu kali

Alisema kuwa alihofia kuwa angepokonywa watoto wake na ndio sababu kuu ya kuficha mimba yake.

Mahakama ilifahamishwa kuwa mwanamke huyo alimnyonyesha mtoto wake kabla ya kumtelekeza katika bustani.

Hata hivyo mtoto huyo tangu kuokolewa , anaishi katika makao ya kuwahifadhi watoto.