Arusha:Wawili wakamatwa na Polisi

Watu wawili wanazuiliwa na Jeshi la Polisi nchini Tanzania wakihusishwa na shambulio la bomu mjini Arusha Tanzania.

Polisi wamewakamata watu wawili wakihusishwa na shambulio hilo lililotokea kwenye mgahawa wa 'Vama Traditional Indian cuisine' jijini Arusha Kaskazini mwa Tanzania.

Shambulizi hilo lilitokea siku ya Jumatatu saa nne usiku.

Watu wasiojulikana walirusha bomu ndani ya mgahawa kupitia mlangoni ambapo watu wanane wamejeruhiwa mmoja kati yao akiwa na majeraha makubwa.

Aidha,katika matukio mengine, jumla ya Watu 20 wanazuiliwa na Polisi wakiwemo watu sita wanaosadikiwa kujihusisha na mlipuko wa bomu uliotokea mkoani Arusha juma lililopita nyumbani kwa Kiongozi wa dini Sheikh Sudi Ally Sudi na kujeruhi watu wawili.

Polisi wanaendelea na upelelezi kuhakikisha inawatia nguvuni watu waliohusika na matukio hayo.