Obama aomba msaada wa dharura

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Obama ameelezea tatizo la uhamiaji kuwa janga

Rais Obama anaomba dola bilioni 3.7 za msaada wa dharura kutoka bunge la Marekani kusaidia kukabiliana na ongezeko la watoto waliohama peke yao kutoka Amerika ya kati.

Ikulu ya Marekani inasema fedha hizo zitasaidia kupunguza kile maafisa wanakitaja kuwa hali ya dharura ya kibinaadamu iliyoshuhudia watoto zaidi ya elfu hamsini na mbili waliohama peke yao kutoka El Salvador, Guatemala na Honduras kuvuka kiharamu mpaka wa Marekani tangu mwezi Oktoba mwaka jana.

Umaskini na ongezeko la hivi karibuni la ghasia zinazohusiana na magenge na mitandao ya ulanguzi madawa ya kulevya zimesababisha ongezeko la wahamiaji kutoka eneo hilo la Amerika ya kati.

Wengi wao watoto ambao wameingia Marekani kupitia bonde la Rio Grande huko Texas.

Wengi wanazuiwa katika vizuizi vilivyo jaa watu wakati maafisa wanang'ang'ana kukabiliana nao.

Rais Obama ameielezea hali kuwa mzozo wa kibinaadamu na sasa anaomba mabilioni ya dola kutoka bunge nchini humo kuharakisha kushughulikiwa na kusafirishwa kwa wahamiaji hao, vile vile kuongeza ukaguzi na kuyasaka makundi ya kihalifu yanayosaidia kusafirishwa kiharamu kwa wahamiaji katika mpaka.

Kampeni katika vyombo vya habari katika nchi wanazotoka wahamiaji hao, inatarajiwa pia kuondosha fikra kwamba watoto wanaowasili Marekani kiharamu wataruhusiwa kukaa.

Licha ya makubaliano kwamba mfumo huo unahitaji mageuzi ya dharura, bunge limetatizwa na iwapo wabadilishe mfumo mzima wa uhamiaji nchini.