UN - Gaza inatishiwa kuangamizwa

Image caption Ban Ki Moon wa umoja wa mataifa

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa, Ban Ki-moon, ameonya kuwa hali huko Gaza imo ukingoni na huenda ikawa mbaya kiasi cha kutoweza kudhibitiwa.

Bwana Ban amesema eneo hilo haliwezi kuhimili vita vingine na ametoa wito kwa pande zote zisitishe ghasia.

Amelitaka kundi la Hamas lisite kufyetua makombora dhidi ya Israel na ameiomba serikali ya Israel kujizuia na iheshimu jukumu lake la kimataifa la kuwalinda raia.

Katibu huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa amepangiwa kufanya mkutano wa dharura Alhamisi na baraza la Usalama la Umoja huo kujadili mzozo wa Gaza.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Benjamin Netanyahu , waziri mkuu wa Israel

Awali, waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alitoa onyo kuwa nchi yake iko tayari kuimarisha oparesheni zake dhidi ya kile alicho kitaja kuwa uvamizi wa kigaidi ndani ya Gaza.

Alitaka mashambulio ya makombora yasitishwe mara moja hidi ya ardhi yake.

Idadi ya makombora inatia hofu

Msemaji mmoja wa jeshi la Israel amesema kuwa zaidi ya makombora 100 yamerushwa kutoka Gaza ambapo 80 kati yao yamelipua ardhi ya Israel.

Maafisa wa matibabu nao wamesema kuwa zaidi ya Wapalestina 60 wameuawa wengi wao wakiwa raia, ndani ya Gaza tangu Israel ianze mashambulio siku ya Jumanne.