Aliyedhani kupona UKIMWI augua tena

Haki miliki ya picha ThinkStock
Image caption Virusi vya HIV

Mtoto mmoja nchini Marekani ambaye alidhaniwa kuwa mtu wa kwanza nchini humo kutibiwa virusi vya HIV akiwa mtoto, amepatikana tena kuwa na virusi hivyo.

Mtoto huyo mwenye umri wa miaka minne kutoka jimbo la Mississipi amekuwa bila ya virusi hivyo kwa zaidi ya miaka miwili baada ya kupata matibabu maalum akiwa bado mtoto mdogo.

Kisa chake kiliibua matumaini makubwa ya tiba ya ugonjwa wa ukimwi.

Madaktari wanasema kuwa kuibuka tena kwa virusi hivyo kumewasikitisha sana.

Madaktari walimpima mtoto huyo na kugundua kuwa angali ameambukizwa virusi vya HIV.

Mwezi Machi mtoto huyo alipopimwa hakupatikana na virusi ikizingatiwa kuwa hakuwa anapokea matibabu kwa karibu miaka miwili.

Bila shaka taarifa hii ni pigo kwa matumaini ya matibabu kutoweza kumaliza virusi vya HIV mwilini kabisa.