Uwanja wa ndege washambuliwa Libya

Haki miliki ya picha AFP

Uwanja wa kimataifa wa ndege nchini Libya umeshambuliwa kwa roketi, siku moja baada ya mapigano kusababisha uwanja huo kufungwa.

Mtu mmoja amefariki huku ndgege 12 zikiharibiwa vibaya katika uwanja huo mjini Tripoli.

Msemamji wa serikali anasema kuwa Libya inatafakari kuomba msaada wa kimataifa kuweza kudhibiti ulinzi.

Viongozi wanakabiliwa na wakati mgumu kurejesha utulivu nchini humo tangu hayati Muamar Gaddafi kuondolewa mamlakani na kisha kuuawa mwaka 2011.

Vurugu zinasemekana kusababishwa na makundi ya wapiganaji wanaopigania mamlaka.

Haijulikani ni kundi gani lililosababisha shambulizi hilo.

Mnamo siku ya Jumapili, kundi moja la wapiganaji lilijaribu kuchukua udhibiti wa uwanja wa ndege kutoka kwa kundi hasimu la Zintan ambalo limekuwa na udhibiti tangu Gaddafi kuondolewa mamlakani.

Duru za usalama zinasema kuwa uwanja huo ulishambuliwa kwa makombora ikiwemo yale ya Grad Jumatatu jioni.

Safari zote za ndege kutoka na kuingia katika uwanja huo zimesitishwa hadi Jumatano.