Tunisia yaomboleza mauaji ya wanajeshi

Image caption Jeshi la Tunisia likishika doria mpakani

Tunisia imesema kuwa takriban wanajeshi wake 14 wameuawa na wengine 20 kujeruhiwa katika shambulizi la wanamgambo karibu na mpaka na Algeria.

Maafisa wanasema wapiganaji waliojihami na makombora walishambulia vizuizi viwili vya kijeshi katika eneo la mlima Chaambi.

Jeshi la Tunisia limekuwa likitekeleza oparesheni zake katika eneo hilo ili kujaribu kuwatimua wanamgambo wanaojificha katika eneo hilo.

Inaarifiwa kuwa idadi kubwa ya vifo vya wanajeshi nchini humo tangu kujipatia uhuru mwaka 1956.

Jeshi la Tunisia limekuwa likifanya operesheni dhidi ya wanamgambo, katika eneo hilo la milimani ,mwaka jana.

Wapiganaji wa kiisilamu wenye uhusiano na kundi la al-Qaeda, wanaaminika kujificha katika eneo la mpakani mwa nchi hiyo.

Wanajesh hao, walishambuliwa na makundi ya wapiganaji Jumatano jioni walipokuwa wanafuturu.

Kundi la wapiganaji lijulikanalo kama 'Okba Ben Nafaa Brigade' , limekiri kufanya mashambulizi hayo kupitia ukurasa wao wa Facebook.

Serikali imetangaza siku tatu za maombolezi, kuanzia leo Alhamisi.

Wanajeshi wanane waliuawa katika shambulizi sawa na hili mwezi Julai mwaka 2013 , siku nyingi tu kabla ya mauaji ya mwanasiasa Mohamed Brahmi, ambayo yaliitumbukiza nchi hiyo katika mgogoro mpya wa kisiasa.