Wapalestina wengi wauawa Gaza

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mmoja kati ya majeruhi wa mapigano eneo la Gaza

Kumetokea vifo vingi katika eneo la Gaza kwa siku moja tangu kuanza kwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Palestina mapema mwezi huu.

Wapalestina zaidi ya sitini kati yao wameuawa kwa kurushiwa mabomu katika mtaa wa watu wengi wa Shejaiya moja ya vitongoji vya jiji la Gaza.

Israel inasema imewapoteza wanajeshi wake 16 katika mapigano hayo.

Kundi la wapiganaji la Hamas wamesema linamshikilia askari mmoja wa Israel huku Jeshi la Israel likisema linaifuatilia taarifa hiyo.

Nyumba nyingi katika Shejaiya zimeachwa zikiwa kifusi kwa kupigwa mabomu na maelfu ya wakazi wamelazimika kuyahama makazi yao.

Zaidi ya wapalestina 420 wameshauawa tangu kuanza kwa mashambulizi yanayofanywa na Israel kwa siku 13 sasa huku Israel ikiwa imeshapoteza watu 20 kati yao raia wawili.

Kupitia katika Televisheni ya taifa, Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema mashambulizi dhidi ya Gaza yataendelea kadri itakavyowezekana ili kuurejesha hali ya usalama Israel.

Katika mazungumzo ya simu, Rais Barack Obama wa Marekani amemwambia Netanyahu kuwa ni haki ya Israel kujilinda lakini akaonya juu ya kuongezeka kwa madhara ya mapigano hayo ikiwamo majeraha na vifo.

Rais Obama anamtuma John Kerry waziri wake wa mambo ya nje kuelekea Cairo katika mazungumzo ya kusitisha mapigano.

Alipokuwa Doha, Qatari, Kerry alilaumu hatua ya Israel na akasema inahatarisha amani ya eneo zima.