Boko Haram washutumiwa kulipua Daraja

Haki miliki ya picha afp
Image caption Wanamgambo wa Boko haram ni tishio kwa usalama wa Nigeria

Wanamgambo wa kiislamu Boko Haram wanashukiwa kulipua daraja kuu kaskazini Mashariki mwa Nigeria na kusababishia dosari usafiri wa kuunganisha nchi hiyo na Cameroon,wakazi wa eneo hilo wameeleza.

Magari na malori yenye mizigo yameonekana kutokua na mwelekeo katika makutano ya barabara yenye kuunganisha daraja la Ngala, BBC imeelezwa.

Siku ya jumanne, mkuu wa majeshi Luteni Jenerali Kenneth Minimah alisema baadhi ya wanajeshi waliondoka wakilihofia kundi la wanamgambo Boko Haram.

Mwandishi wa BBC, mjini Abuja anasema kuwa jeshi la Nigeria limekosa nguvu kutokana kukosa motisha ambayo ingewapa nguvu ya kupambana na Boko Haram.

Hali hii imejitokeza ingawa jeshi la nchi hiyo ni kubwa zaidi Afrika magharibi, na limekuwa likipambana na makundi mbalimbali ya wanamgambo katika nchi kadhaa kama vile Sierra Leone kukomesha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan alitangaza hali ya hatari zaidi ya mwaka mmoja uliopita katika majimbo ya Borno, Yobe na Adamawa akiahidi kulipa nguvu zaidi jeshi lake kupambana na Boko Haram.

Waangalizi wa haki za binaadam wamesema kuwa takriban watu 2,053 wameuawa kwenye mashambulizi takriban 95 katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2014, ikilinganishwa na idadi ya vifo 3,600 katika kipindi cha miaka mine ya kwanza ya mgogoro.