Ajali yaua watu 17 Tanzania

Haki miliki ya picha MADHUSUDAN
Image caption Moja ya ajali ya magari ya abiria

Watu 17 wamekufa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea mkoa wa Dodoma katikati mwa Tanzania.

Taarifa zinasema ajali hiyo imetokea baada ya magari mawili, moja lori na jingine basi la abiria kugongana uso kwa uso.

Akizungumza na BBC Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma David Misime amesema ajali hiyo iliyotokea majira ya saa mbili za asubuhi siku ya jumatano imesababishwa na kile kinachodaiwa kuwa uzembe wa dereva la gari moja lililohusika katika ajili hiyo.

Amesema ajali hiyo ilihusisha basi la abiria na Lori ambayo yaligongana uso kwa uso baada ya dereva wa lori kujaribu kulipita gari jingine bila kuangalia vizuri na hivyo kujikuta yakigongana.

Tayari polisi wa Tanzania wameanza uchunguzi ili kujua chanzo cha ajili hiyo lakini hata hivyo imeshindwa katika hatua za awali kumshikilia mtu yoyote kwa vile maderava na magari yote ni miongoni mwa walikufa katika ajali.

Hii si mara ya kwanza kwa ajali kama hii kutokea hapa Tanzania ambapo sababu kadhaa zimekuwa zikitajwa kusababisha ikiwemo mwendo kasi wa magari, uzembe wa madereva, pamoja na ubovu wa barabara