Ban alaumu mashambulizi ya shule

Haki miliki ya picha AP
Image caption Katibu mkuu alalamikia Israeli kuhusu Mashambulizi ya majengo yake.

Katibu Mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-Moon amelaumu mashambulizi ya Israel dhidi ya Shule ya Umoja wa Mataifa iliyoko Gaza ambako maelfu ya Wapalestina walikuwa wamejihifadhi kukwepa mashambulizi.

Ban Ki moon amesema hakuna kitu cha aibu kama kushambulia watoto waliolala. Amesisitiza uwajibikaji kwa waliofanya kitendo hicho kilichowaua watu 15 na kuwajeruhi wengine kadhaa.

Marekani nayo bila kuitaja waziwazi Israel wamelaumu kitendo hicho. Hata hivyo msemaji wa Jeshi la Israel Luteni Kanali Peter Lerner amesema lilikuwa tukio la kuumiza mno.

Image caption Ban anasema kuwa Israeli ilikuwa inajua kuwa shule hiyo ni ya UN

Msemaji kimataifa umoja wa mataifa Chris Gunness amesema kitendo hicho cha jeshi la Israel hakiwezi kuwa na sababu ya kujitetea tunalaani vikali ukiukwaji huu wa sheria za kiamataifa zilizofanywa na majeshi ya Israel kwa sababu uchunguzi tuliofanya umeonyesha kwamba wanahusika.

Tulishalionya jeshi la Israel mara 17, tuliwaambia kwa hakika shule ilipo, tukawaambia ilikuwa imejaa zaidi ya watu 3000 ambao walikimbilia mapigano.

Kamishina Pierre Kraehenbuehl amesema shule ilikuwa imehifadhi raia ambao hawakuwa na mahali pa kwenda.