Waaga dunia pamoja baada ya miaka 62

Image caption Don na Maxine Simpson wakiwa hospitalini

Amini Usiamini mapenzi ya kweli bado yapo humu duniani!

Kisa kimoja ambacho kimedhibitishia wengi baada ya wapenzi wawili waliooana na kuishi pamoja kwa takriban miaka 62 walipoaga dunia pamoja.

Don na Maxine Simpson walikuwa wakazi wa mji wa Bakersfield, ulioko jimbo la California, Marekani waliaga dunia saa nne baada ya kushikana mikono hospitalini na kuahidiana penzi lao halitafifia kamwe hata mauti iwapate.

Walikuwa wamelazwa hospitalini kufuatia hali duni ya afya inayotokana na umri wao mkubwa.

Image caption Don na Maxine Simpson wakiwa bukheri wa afya

Lakini punde alipoaga Maxine na mwili wake ukaondolewa chumbani walikokuwa wamelazwa pamoja na mumewe Don, zilipata saa nne tu uchungu ulipomzidi Don na akakata roho iliwaendelee kupendana na mkewe ahera.

Mjukuu wao Melissa Sloan aliiambia runinga ya KERO-TV Kuwa Don alimhusudu sana nyanya yake yaani Maxine tangu alipomtupia jicho mnamo mwaka wa 1952 walipokutana katika mashindano ya Bowling.

Wapenzi hao wawili waliooana mwak huohuo na hawajawahi kuachana tangu hata katika mauti.

''Babu yangu alikuwa anatamani kuishi na nyanya yangu na hata baada ya wawili hao kuanza kuugua kutokana na umri wao mkubwa waliwaomba wasimamizi wa hospitali walimolazwa wasiwatenge.''

Don alikuwa na miaka 90 huku mke wake akiwa na miaka 87.

Image caption Don na Maxine Simpson walipokutana

''Babu yangu alihudumu kama mwanajeshi katika jeshi la Marekani naye bibi alikuwa ni muuguzi haswa walipokuwa huko Ujerumani ambapo waliwahi kuishi kwa muda mrefu.''alisema mjukuu wao Melissa.

Wamemuacha nyuma mtoto mmoja wa kiume na wajukuu watano.

Je unaamini kuna penzi la kweli ?

Tuwachie jibu lako katika mtandao wetu wa facebook BBCSwahili.com na pia kwenye tweeter @bbcswahili.