Kifo cha pili kutokana na Ebola Nigeria

Nigeria imeripoti kifo cha pili kutokana na homa kali ya Ebola ambayo imekuwa janga kubwa katika kanda ya Afrika Magharibi.

Inaarifiwa muuguzi mmoja amefariki huku watu wengine 5 wakithibitshwa kuambukizwa ugonjwa huo. Taarifa hii ni kwa mujibu wa waziri wa afya nchini humo Onyebuchi Chukwu.

Muuguzi huyo alimtibu mwanamume aliyekuwa anaugua Ebola ingawa alifariki mwezi jana.

Alisema kuwa watu watano wanaothibitishwa kuwa na ugonjwa huo wanatibiwa mjini lagos, mji mkubwa wenye idadi ya watu milioni 21.

Watano hao walioambukizwa wanasemekana kuambukizwa na Patrick Sawyer ambaye aliugua baada tu ya kutua mjini Lagos na kufariki siku tano baadaye.

Maafisa sasa wanafuatilia watu wengine kuona ikiwa wana dalili za homa hiyo kali.

Chukwu alisema maafisa wanabuni kituo cha dharura cha kukabiliana na ugonjwa huo, ambacho kitaanza kutumika mnamo Alhamisi.

Waziri aliongeza kwamba vituo maalum vitatengwa kwa ajili ya kuharakisha maeneo maalum ya kutengewa wagonjwa katika majimbo yote nchini humo.