KQ kuendelea na safari Afrika Magharibi

Image caption Kenya Airways kuendelea na safari zake Magharibi mwa Afrika

Shirika la ndege la Kenya, Kenya Airways limetangaza kuwa litaendelea na safari zake za ndege kama kawaida kuelekea magharibi mwa Afrika, licha ya mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.

Katika taarifa yake ya hivi punde afisa mkuu mtendaji wa shirika hilo, Titus Naikuni, amesema kuwa shughuli za usafiri zitaendelea.

Aidha Shirika hilo linaendelea kushauriana na mashirika ya afya ya umma kama vile shirika la afya duniani , WHO na shirika la kimataifa la usafiri wa ndege I-A-T-A kutathmini athari iliyopo.

Taarifa hiyo pia imesema kuwa abiria wote kutokea eneo la Magharibi mwa Afrika watafanyiwa uchunguzi wa kina pindi wanapotua katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi kabla ya kuruhusiwa kuabiri ndege za kuelekea mataifa mbalimbali .

Haki miliki ya picha EPA
Image caption KQ inasema kuwa inafuata ushauri wa WHO

Licha ya kuwa mashirika tofauti ya ndege yamefutilia mbali safari zao kuelekwa Magharibi mwa Afrika Kenya Airways imesema kuwa itaendelea kuwasafirisha abiria licha ya milipuko ya Ebola.

Kenya Airways inasema imechukua hatua hiyo kufuatia tangazo la shirika la Afya Duniani, WHO, kuwa uwezekano wa abiria kuambukizwa maradhi kwa kutembelea eneo hilo tu ni duni sana.

Kampuni ya Kenya Airways inasema kuwa imewahamasisha wafanyakazi wake wote kuhusiana na jinsi maradhi hayo ya Ebola yanavyoambukizwa na kuwa wamepewa vifaa vya kinga.

Wizara ya Afya ya Kenya ilitangaza juma lililopita kuwa haitaunga mkono mapendekezo ya kuweka vikwazo vya kibiashara au usafiri kwa eneo linalotajwa kuwa na virusi vya maradhi hayo.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption KQ kuendelea na safari Afrika Magharibi

Shirika la Kenya Airways linasema kuwa kuondoa ndege zake kutoka safari za Afrika Magharibi itamaanisha kuwa shirika linachangia katika kuweka vikwazo vya safari.

Watu wote walioambukizwa virusi vya Ebola nchini Nigeria wamethibitishwa kuwa waligusana na mtu aliyetua Lagos kutoka Monrovia na baadaye akafariki.

Shirika la ndege la Uingereza, British Airways, limesitisha ndege zake kwenda Lagos na Monrovia hadi mwisho wa Agosti.

Zaidi ya watu 930 wameaga dunia nchini Sierra Leone, Liberia, Guinea na Nigeria katika kile kinachotajwa kuwa mlipuko mbaya zaidi wa ugonjwa wa Ebola kuwai kushudiwa.