Obama atetea Marekani kushambulia ISIS

Wayazidi wakikimbilia Irbil, mji mkuu wa jimbo la Wakurd, kaskazini mwa Iraq Haki miliki ya picha AP

Rais Obama amesema hataruhusu wapiganaji wa siasa kali wa madhehebu ya Sunni kuunda himaya yao nchini Syria na Iraq; na ndege za Marekani zitafanya mashambulio zaidi ikihitajika.

Rais Obama aliliambia gazeti la New York Times, ni masilahi ya Marekani kuwazuwia wapiganaji wa ISIS wasisonge mbele na piya ina wajibu kuzuwia mauaji ya kimbari.

Katika hotuba yake ya kila juma, alisema wapiganaji hao wanawateka wanawake na kuwafanya watumwa wao na wanatishia kuiangamiza jamii ya madhehebu ya Yazidi yenye waumini wachache.

Alisema mashambulio ya ndege yanaweza kumaliza kuzingirwa kwa wakimbizi wa Yazidi waliokimbilia milimani.

Ndege za Marekani kwa mara ya pili zimedondosha msaada wa dharura kwa maelfu ya wakimbizi wa madhehebu ya Yazidi ambao wamenasa mlimani, kaskazini mwa Iraq.

Walikimbia makwao wakati wapiganaji wa ISIS walipokaribia.