US:Wapiganaji wa Islamic state ni tisho

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Chuck Hagel na generali Dempsey wakihutibia wahabari

Marekani imesema kuwa kundi wapiganaji wanamgambo wa Islamic State( IS) ni hatari kwa usalama wa mataifa mengi katika kanda ya Mashariki ya Kati na washirika wake katika Mataifa ya Magharibi.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Chuck Hagel, amewataja wapiganaji hao wa IS kuwa kundi lisiloeleweka na linazidi kundi lingine lolote lile la kigaidi.

Hata hivyo hakuna kilichosemwa kuhusu hatua ilizochukuliwa na jeshi la Marekani zaidi ya mashambulizi ya angani yaliyoagizwa na Rais Obama.

Marekani imeanza uchunguzi wa mauaji ya kikatili ya mwanahabari wa nchi hiyo , James Foley, na wapiganaji wa Kiislamu.

Kundi hilo limechukua sehemu kubwa ya Iraq

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Marekani kuishambulia IS zaidi

Bwana Hagel ameonya kuwa kundi hilo lililoteka sehemu kubwa ya kaskazini mwa Iraq na sehemu ya Syria lazima likabiliwe vilivyo ilikuepusha Marekani na uharibifu.

Amiri jeshi wa Marekani Martin Dempsey naye ameonya kuwa lazima kikundi hicho kikavamie katika makao yake makuu huko Syria.

Bwana Hagel amedhibitisha kuwa makomando wa jeshi la Marekani walijaribi kumuokoa mwandishi wa kimarekani lakini wakashindwa.

Wapiganaji hao wa IS walikuwa wameitisha dau la dola milioni 132 ilikumuachilia huru mwandishi huyo wa habari.

Generali Dempsey alisema kuwa kundi hilo linaufadhili unaozidi matarajio ya Wamarekani na kuwa linauwezo mkubwa wa kijeshi baada ya kuteka silaha walizowapokonya majeshi ya wamarekani mbali na silaha walizotwaa walipoteka kambi mbili za majeshi ya Iraq kaskazini mwa taifa hilo majuzi.

Aidha Jeshi hilo liliteka kambi ya jeshi la Syria vilevile na kujizolea silaha za kisasa.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Viongozi wa kundi la Islamic State .

''hilo ndilo tatizo letu wanapesa kutokana na uporaji wa mabenki uuzaji wa mafuta kaskazini mwa Iraq mbali na wafadhili katika mataifa ya Ghuba.

Ni lazima tutakabiliana nao ikiwa si sasa muda utawadia tu.''

hata hivyo wadadisi wa maswala ya Iraq walisema kuwa wote wawili hawakutangaza badiliko la kampeini yao huko Iraq.

Mapema wiki hii rais Obama alikuwa amesema kuwa wataishambulia IS bila ya kutuma wanajeshi wa nchi kavu Iraq lakini inavyoelekea sasa huenda Marekani ikaanza kupanga mikakati ya kuinyamazisha IS nchini Iraq na pia Syria