Meneja redio Shabelle yuko mafichoni’

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Abdimalik Yusuph na Mohamed Bashir mwandishi wa habari wakiwa mahakamani

Meneja wa redio Shabelle, inayomilikiwa kibinafsi, iliyoko Mogadishu, mji mkuu wa Somalia, amearifu BBC kuwa yuko mafichoni baada ya utawala nchini humo kuifunga stesheni yake.

Mohamed Musa amesema wanajeshi walishambulia ofisi za stesheni hiyo siku ya Ijumaa, na kutia watu 20 nguvuni, watatu kati yao wakiwa wamezuiliwa hadi sasa bila ya kufunguliwa mashtaka.

Redio hiyo ilirejea kupeperusha matangazo yake siku ya Jumanne, lakini ilivamiwa tena na vifaa vyote vya utangazaji kutolewa.

Musa amekana madai kuwa redio hiyo ilikuwa inaeneza habari zinazochochea chuki.

Serikali, inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, ilitoa habari inayosema kuwa stesheni hiyo haikufuata sera za taaluma ya utangazaji kwa kueneza ujumbe unaochochea vurugu kati ya jamii za Mogadishu.

‘Jambo la kutisha’

HALI IKOJE MOGADISHU?

Kumekuwepo na wasiwasi mjini Mogadishu kufuatia operesheni ya serikali ya kupokonya raia silaha zisizo halali, ambapo wanamgambo katika vitongoji kadhaa wamepokonywa silaha.

Bwana Musa amesema Shabelle haikupeperusha habari zozote za kuegemea upande mmoja, zinazounga mkono au dhidi ya operesheni hiyo ya serikali.

"Hatuegemei upande wa serikali, hatuegemei upande wa wapinzani, sisi hupasha wanachi yaliyo ya kweli,” aliarifu BBC Focus katika kipindi cha redio cha Afrika.

Mwanahabari wa BBC Mohammed Moalimu aliye Mogadishu amesema mashirika ya watangazaji yamekashifu kukamatwa kwa watangazaji hao na kuelezea kushtushwa kwao na mkondo unaochukuliwa na serikali katika operesheni zake.

Kumekuwepo na miito ya wanahabari waliokamatwa kufunguliwa mashtaka kulingana na katiba, kwani katiba inaelekeza kuwa waliozuiliwa hufaa kufikishwa mahakamani kwa kipindi cha masaa 24.

UHUSIANO WA SERIAKALI NA KITUO HICHO UKOJE?

Bwana Musa alikiri kuwa kulikuwepo na uhusiano wa kiuhasama kati ya Shabelle na serikali, mwaka uliopita redio hiyo ilikuwa mpangaji katika jumba la serikali, na serikali iliwafukuza kutoka humo.

Musa alisema aliamini kuwa amri ya kukamatwa kwake ilikuwa imetolewa na alihofia kuwa huenda wanahabari wenzake waliotiwa nguvuni wakatendewa unyama.

"Niko mafichoni Mogadishu.... Nahamahama, ni jambo la kutisha mno."

Wababe wa vita vya kiukoo, wanasiasa hasimu, na wanamgambo wa kiislamu wamekuwa wakipigania uthibiti wa Somalia tangu Siad Barre kuondolewa mamlakani 1991 baada ya kuongoza kwa muda mrefu.

Chini ya mpango unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, serikali mpya ilibuniwa mwaka 2012 inayojaribu kuchukua uthibiti wa maeneo yaliyochukuliwa na wanamgambo wa Al-Shabaab walio na mtandao na al-Qaeda, ili kurejesha utulivu nchini humo wakisaidiwa na Umoja wa Afrika.